UTANGAZAJI KUWAENDEA MASTAA NA WACHEKESHAJI, WASOMI WENYE SHAHADA ZA FANI HIYO WANAJIFUNZA NINI

Umesoma utangazaji kwenye chuo kikubwa chenye sifa na umepata shahada au stashahada yako, lakini hadi leo, unazunguka na bahasha ya kaki mkononi yenye vyeti vyako, kutafuta kazi lakini nazo zimeota mbawa! Kazi ngumu, ngumu kweli kweli kupata.

Umetuma CV yako kwenye vituo vya redio kibao, lakini hujaitwa hata kwenye usaili, na kama uliitwa, hukupata kazi. Inauma kwasababu, umesota miaka mitatu ukiusomea utangazaji na kozi zingine kibao zilizokufanya ujiamini kusimama mbele ya wenye weledi katika fani hiyo. Mtihani mkubwa!

Lakini unashangaa video vixen mwenye skendo lukuki, Gigi Money anapata kazi kwa ulaini kabisa na kupewa kipindi chake. Ahh, hadi leo anakula matunda ya umaarufu wake wa Instagram!

Unaduwaa, wachekeshaji MC Pilipili na Mpoki wakipewa kazi kama kumsukuma mlevi na mshahara mnono. Kama hiyo haitoshi, unaduwaa zaidi, mchekeshaji mwingine, Kicheko anapokelewa kwa ndelemo na vifijo kwenye redio yenye ushawishi mkubwa nchini, Clouds FM na mapokezi yake yanarushwa live!

Wewe mwenzangu na mimi uliyeisotea shahada ya utangazaji ukiendelea kupiga kwata, kuchomwa jua la utosi, kiguu na njia kutafuta kazi ya utangazaji na unachokutana nacho ni kibuti tu!
Ni ukweli unaouma kuwa tasnia ya utangazaji haijali tena vyeti vyako! Hii haipo Tanzania peke yake. Kenya ndio kabisaaa, redio zimejaa wachekeshaji, watu waliokuwa kwenye muziki ama watu maarufu kwa vyovyote vilivyowafanya wawe hivyo.

Katika semina moja ya Fursa, mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, alisema ana angalau miaka mitatu, hajawahi kusoma CV ya mtu anayeomba kazi. Anachoangalia zaidi ni nini unachoweza kufanya, uwe umeishia darasa la saba au umehitimu shahada – kama unaliwezea gunzi, basi mzigo unapata!
Mahitaji ya mtangazaji wa redio wa Tanzania katika zama hizi za leo, ni sauti nzuri, kipaji halisi cha kutangaza na siku hizi umaarufu na ushawishi wako.

WEWE MWENYE SHAHADA UNAPASWA KUJUTA KWA CHAGUO LA ELIMU YAKO?
Kwa hali ilivyo sasa, sitoshangaa ukijilaumu kutumia miaka mitatu kusomea utangazaji. Ni kwasababu asilimia kubwa ya wahitimu wa fani ya mawasiliano ya umma ambayo hubeba utangazaji, uandishi wa habari na uhusiano wa umma (public relations), huishia kufanya kazi zingine kabisa.

Wengi utawakuta kwenye mabenki, mashirika ya umma, kampuni binafsi na sehemu zingine wakifanya kitu tofauti kabisa na walichosomea. Ni kwasababu kwanza, kazi za utangazaji kwa Tanzania hazina mishahara mikubwa kama unavyodhani. Wanaolipwa fedha nyingi ni wale wenye ushawishi, wenye majina, bila kuzingatia viwango vyao vya elimu. Na pia viwango vya mishahara vinapishana kwa ukubwa kulingana na redio husika.

KUNA MATUMAINI LAKINI..
Pamoja na changamoto hizo, hupaswi kukata tamaa. Elimu haijawahi kuwa laana – elimu ni baraka siku zote. Hivi karibuni kumekuwepo na ‘concern’ ya umuhimu wa waandishi wa habari na watangazaji kuwa weledi. Kwa maana kuwa, itafika siku, makampuni yataanza kuzingatia elimu za watu wanaowaajiri, yakitarajia kupata kitu sahihi.

Hiyo inabidi iwe changamoto kwa wasomaji wa fani ya habari kwa kuhakikisha wanafanya vitu tofauti, kwendana na elimu zao. Kama una shahada ya utangazaji, hakikisha unapowasha kinasa sauti kuongea, msikilizaji anakutofautisha na mwingine asiye na elimu yako kwa kile tu unachozungumza.

Kwa kufanya kazi kwa mazoea, si rahisi thamani yako kuonekana, na nafasi hizo zitajazwa na vijana wenye vipaji na wanaojituma bila kuwa na elimu yoyote ya masuala hayo.
       
BY FREDRICK BUNDALA

No comments

Usisaau ku like